- Posted by:
- Posted on:
- Category:
ElimuElimu - System:
Unknown - Price:
USD 0
Mwongozo huu wa upimaji umeandaliwa kwa lengo la kuwajengea uwezo walimu wanaofundisha Shule za Msingi kuhusu namna ya kuboresha upimaji katika mchakato mzima wa ufundishaji na ujifunzaji. Mwongozo huu unaonesha namna upimaji wa maendeleo ya wanafunzi unavyotakiwa kufanyika ili kupata matokeo yanayoakisi uwezo halisi wa mwanafunzi.
Aidha, unaelezea dhana ya upimaji, malengo, aina na hatua za upimaji. Pia unaeleza namna bora ya kufanya ufuatiliaji na tathmini ya upimaji.Vile vile mwongozo unafafanua misingi ya uandaaji wa maswali bora ya upimaji na ufanyikaji wa upimaji. Zaidi ya hayo, mwongozo umebainisha mbinu za usahihishaji wa upimaji na utunzaji wa alama za wanafunzi zinazotokana na upimaji/mtihani husika.
Kwa kuzingatia vigezo vya upimaji vilivyobainishwa katika mwongozo huu, mwalimu ataweza kufanya upimaji kwa kutumia vigezo stahiki vitakavyomsaidia kupata matokeo yanayoendana na uwezo wa kila mwanafunzi. Vigezo hivyo ni kama vile; kuandaa jedwali la upimaji, kutunga aina mbalimbali za maswali yenye ubora unaolingana na ngazi ya elimu ya Msingi, kuendesha na kusahihisha upimaji kwa kufuata utaratibu unaotakiwa pamoja na kurekodi na kutunza alama za matokeo ya upimaji wa somo husika.
Upimaji
Upimaji katika elimu ni kitendo endelevu cha kutafuta ni kwa kiasi gani mwanafunzi amepata maarifa au stadi zilizofundishwa kwa kuzingatia malengo ya ufundishaji na ujifunzaji wa vipengele mbalimbali vya umahiri kama vilivyobainishwa kwenye muhtasari wa somo husika.
Pia, upimaji hujumuisha mwenendo, tabia na uwezo wa mwanafunzi wa kufanya mambo mbalimbali.
Malengo ya Upimaji
Mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji hauwezi kukamilika bila kufanya upimaji. Upimaji hufanyika ili:
- Kubaini kiwango cha uelewa kilichofikiwa na wanafunzi baada ya kufundishwa na kujifunza maudhui/mada mbalimbali;
- Kufuatilia maendeleo ya mwanafunzi katika mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji. Matokeo ya upimaji humsaidia mwalimu kuboresha mbinu, njia na zana anazotumia katika ufundishaji iwapo wanafunzi wake watakuwa wamepata ufaulu wa chini. Aidha, wanafunzi wataona umuhimu wa kuongeza juhudi katika ujifunzaji;
- Kubaini matatizo ya mwanafunzi katika kujifunza. Matokeo ya upimaji humsaidia mwalimu kufanya uchunguzi yakinifu na kubaini changamoto inayosababisha wanafunzi kufanya vibaya, hatimaye kugundua tatizo na kulitafutia ufumbuzi. Kwa hiyo kutokana na ufaulu wa chini anaoupata mwanafunzi huyo, utamwezesha mwalimu kugundua tatizo na kulitatua;
- Kuandaa vigezo vya kutumia wakati wa kuwapanga wanafunzi katika madaraja kwa kuzingatia viwango vya ufaulu ili kuchagua wanafunzi wanaotakiwa kuendelea na madarasa ya juu na wanafunzi wanaotakiwa kurudia darasa kutokana na kushindwa kumudu umahiri na stadi za ngazi husika.
- Kubaini wanafunzi wenye umahiri wa kuweza kujieleza na kujenga hoja na kujiamini, hivyo kuandaa rasilimali watu wenye ujuzi na weledi wa kuweza kuchangia katika ujenzi wa uchumi wa nchi yao.
- Kuwapa wanafunzi changamoto ya kujifunza na kujenga tabia ya kujisomea zaidi kwani kwa kufanya upimaji wanafunzi watakuwa na ufahamu kuwa baada ya kufundishwa na kujifunza watapimwa.
- Kuwezesha shule husika kujua ufanisi wake katika kutekeleza mtaala wa elimu katika ngazi husika ikilinganishwa na shule nyingine.
- Kuwashauri viongozi wa elimu kuhusu ubora au mapungufu ya mitaala inayotumika.
Soma zaidi: